VIONGOZI IAASO, CRs WAFUNDWA MAADILI YA UONGOZI

 

Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma Kanda ya Kasikazini imetoa mafunzo maalumu ya maadili kwa viongozi wa serikali ya wanafunzi pamoja na CRs.


Katika mafunzo hayo yaliyotolewa Februari 7, 2026 viongozi wameelimishwa mambo mbalimbali ya kimaadili ambayo yakifanywa yanaweza kuharibu taswira na heshima ya chuo na kiongozi binafsi. Vile vile wameelimishwa namna ya kujiepusha na mambo mbalimbali yasiyo ya kimaadili kama mgongano wa masilahi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.


Kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii kama facebook, Twitter (X), Instagram, Youtube na mingineyo, viongozi hao pia wameelimishwa juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii katika kujenga wasifu wao (CV), kujitambulisha katika kile wanachofahamu kitaaluma na kuepuka matumizi mabaya ya mitandao kama kueneza taarifa ambazo hazijathibitishwa.


Halikadharika, katika matumizi ya jina la taasisi (IAA), viongozi hao pia wameonywa dhidi ya matumizi mabaya ya jina la taasisi kwani hupelekea kuvunja heshima ambayo imejengwa kwa muda mrefu. Vile vile Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma Kanda ya Kasikazini imewaasa viongozi kutumia vyema jina la taasisi katika maisha ya mtandaoni na jamii kwa ujumla.


“Ambavyo wewe utajitambulisha huishii kusema John, wewe pia ni mwanafunzi wa chuo maana yake unabeba dhamira mbili yaani dhamira ya kwako na dhamira ya chuo” wamesema.


Wakizungumzia umuhimu wa kutoa elimu kwa wanafunzi wa vyuo Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma Kanda ya Kasikazini imesema ni kuwaandaa kuja kuwa viongozi wazuri na wenye maadili thabiti.


“wewe ni kiongozi wa umma unayetarajiwa, kwaiyo kama Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma tunasimamia maadili ya viongozi, viongozi wa sasa itafika hatua watastaafu nani atachukua hizo nafasi? Si ndio sisi wenyewe tuliopo chuo? Ina maana tutakuja kuwajibika na maadili ya viongozi wa umma.” Wamesema.


Kwa upande wake Nadhiru Abdulnuru, Mkurugenzi wa huduma za wanafunzi ameishukuru Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma Kanda ya Kasikazini kwa kuamua kutoa elimu ya maadili kwa viongozi wa serikali ya wanafunzi IAA, kwani itasaidia kuwajenga na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya kila siku bila ukiukwaji wa sharia na maadili ya uongozi.


Naye, Rais wa Serikali ya wanafunzi-IAASO Francis Wambura pia ameipongeza Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma Kanda ya Kasikazini kwa elimu hiyo, akisema mafunzo hayo ikiwezekana yatolewe kila mwezi kwa viaongozi wa serikali ya wanafunzi na wanafunzi kwa ujumla, ili kuendelea kuwajengea misingi imara ya uongozi wawapo chuoni na hata nje ya chuo.