Usiku wa tarehe 13 Februari, 2026 haukuwa usiku wa kawaida. Ndani ya viwanja vya IAA, anga lilipambwa na mwanga wa taa za rangi, sauti za muziki zikivuma hewani, na shamrashamra za wanafunzi wapya na wakongwe zikichanganyika kwa furaha isiyo kifani. Ilikuwa ni IAA Welcome Freshers’ Party 2025/2026, hafla iliyosubiriwa kwa hamu kubwa na kila mmoja chuoni.
Mapema jioni, ukumbi ulianza
kujaa. Mavazi ya kuvutia, vicheko vya furaha, na picha zisizokoma vilitawala
kila kona. Freshers walikuwa na bashasha nyusoni, wakifurahia kukaribishwa
rasmi katika familia ya IAA. Kadri muda ulivyosogea, shangwe ziliongezeka kila mmoja akisubiri wasanii waliotangazwa
kupanda jukwaani.
Msanii mkubwa Tanzania Chino Kidd. Mara tu alipoanza kutumbuiza, umati ulilipuka kwa
shangwe. Nyimbo zake zilifanya kila mtu asimame, akitingisha miili kwa furaha.
Mwanga wa simu ulijaa hewani, ukitoa mandhari ya kuvutia kana kwamba nyota
zimeshuka ardhini.
Katika usiku huu pia msanii Dogo Janja, alipanda stejini na akaongeza moto wa burudani kwa staili yake ya kipekee. Sauti za mashabiki
ziliimba sambamba naye, na ukumbi mzima ukageuka bahari ya watu waliokuwa
wakicheza bila kuchoka. Nishati ilipanda maradufu.
Balaa MC
alipochukua mic, alihakikisha hakuna aliyebaki amekaa. Maneno yake ya kuvutia
na mawasiliano ya karibu na mashabiki yalifanya kila mmoja ajisikie sehemu ya
show. Usiku huo haukuwa wa kutazama tu, bali wa kushiriki kikamilifu.
Hata hivyo, msanii kutoka Arusha Fido Vato na Lord Eyez waliendelea kuamsha shangwe kwa vibao vyake vilivyopendwa. Hakukuwa na
muda wa kupumzika kila wimbo uliibua nderemo na vigelegele vipya.
Moto uliendelea kuwaka pale Barobaro
alipopanda jukwaani, akifuatiwa Kidensa MC, kila mmoja akileta ladha
yake ya kipekee. Ukumbi mzima ulitikisika kwa midundo mizito na sauti za
furaha. Watu walicheza kwa makundi, wengine wakirekodi matukio ili kuyahifadhi
kama kumbukumbu ya siku hiyo adhimu.
Hatimaye, Dushy Boy akapanda stejini kwa perfomansi iliyowaacha wengi vinywa wazi. Alishirikisha mashabiki wake kwa
karibu, na kila mmoja alihisi kama sehemu ya historia hiyo ya kipekee ya IAA.
Ilipofika usiku wa manane
kuelekea alfajiri, ingawa miguu ilikuwa imechoka, mioyo ilikuwa imejaa furaha.
Freshers walihisi kukaribishwa rasmi katika maisha ya chuo, na wanafunzi
wakongwe walijivunia kuonyesha upendo na mshikamano wao.
Usiku wa tarehe 13 Februari,
2026 uliandikwa katika kurasa za kumbukumbu za IAA kama moja ya hafla zilizofana
zaidi usiku wa muziki, umoja, na mwanzo mpya kwa kizazi kipya cha wanafunzi.













