MSIBANI SONGEA:
Mwili wa marehemu Aneth
Ndunguru aliyekuwa mwanafunzi wa IAA Shahada ya Utalii na Ukarimu mwaka wa tatu
(BACHELOR OF TOURISM AND HOSPITALITY MANAGEMENT WITH APPRENTICESHIP), aliyefariki
dunia Machi 28, 2026, katika hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha alipokuwa
akipatiwa matibabu, umepumzishwa katika makazi yake ya milele huko Ruvuma
wilayani Songea leo April 01, 2026.
Mazishi na shughuli ya kumpumzisha
marehemu Aneth Ndunguru kwenye nyumba yake ya milele yalianza na chakula kwa
watu wote, kuaga mwili wa marehemu, ibada kutoka kwa viongozi wa dini, msafara
wa makaburini uliohusisha watu wote, mazishi, salamu za rambirambi, kutawanyika
makaburini na mwisho wawakilishi kutoka Arusha walianza safari ya kurudi
Arusha.
HISTORIA FUPI YA MAISHA YAKE:
Marehemu ndugu Aneth Stanley Ndunguru alizaliwa tarehe 02 Juni, 2003 katika hospitali ya Ruvuma. Alibatizwa mnamo tarehe 11 April, 2007 katika Parokia ya Songea na kupata sakramenti ya Komunio ya kwanza na Kipaimara mwaka 2015 katika Parokia ya Songea.
Marehemu ndugu Aneth Stanley
Ndunguru alianza safari yake ya elimu ya msingi mwaka 2010 katika shule ya
msingi Mloweka na kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2016. Marehemu ndugu Aneth
Ndunguru alipata nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari kidato cha kwanza
hadi cha nne mwaka 2017-2020 katika shule ya sekondari Londoni na mwaka
2021-2023 akasoma elimu ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari
Chisenga. Na baada ya kumaliza elimu ya juu ya sekondari marehemu Aneth
Ndunguru alijiunga na mafunzo ya mujibu wa sharia ya JKT huko Sumbawanga mkoani
Rukwa.
Mnao mwaka 2023, marehemu
Aneth Ndunguru alijiunga na elimu ya chuo kikuu katika Chuo Cha Uhasibu Arusha-IAA
katika Shahada ya Utalii na Ukarimu (Bachelor Degree in Tourism and Hospitality
Management with Apprenticeship) na mwaka huu 2026 alikuwa akihitimu na
kutunikiwa shahada yake.
KUUGUA:
Marehemu Aneth Ndunguru alianza kuugua siku ya alhamisi tarehe 26 Machi, 2026 akapata dawa za maumivu na kuendelea na mitihani yake ya kumaliza muhula wa kwanza wa mwaka wa masomo 2025/2026 (Semister 1 Examination). Ilipofika Ijumaa 27 Machi, 2026 baada ya kumaliza mtihani wa siku hiyo, hali yake lilibadilika akapelekwa kituo cha afya kilichopo jirani kwa matibabu, kisha kuruhusiwa kurudi nyumbani. Ilipofika saa 2 usiku hali yake ilibadilika na kurudishwa tena kituo cha afya na badae akapewa rufaa kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha na kupelekwa chumba maalum cha wagonjwa mahututi (ICU). Ilipofika tarehe 28 Machi, 2026 umauti ulimfika ndugu Aneth Ndunguru.
KUAGWA
ARUSHA
Machi 30, 2026 ilikuwa ni siku
na wakati wa simanzi na majonzi makubwa Zaidi kwa jamii nzima ya Chuo Cha
Uhasibu Arusha-IAA, katika shughuli ya kuaga na kutoa salamu za mwisho kwa
mwili wa marehemu Aneth Ndunguru aliyekuwa mwanafunzi wa IAA akisoma Shahada ya
Utalii na Ukarimu mwaka wa tatu (BACHELOR OF TOURISM AND HOSPITALITY MANAGEMENT
WITH APPRENTICESHIP), aliyefariki dunia Machi 28, 2026, katika hospitali ya Mount
Meru mkoani Arusha alipokuwa akipatiwa matibabu.
Shughuli ya kuaga mwili iliyoanza majira ya saa 6 mchana iliongozwa na Naibu
Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Dkt. Grace Idinga, na
viongozi mbalimbali wakiwemo Meneja wa IAA-Kampasi ya Arusha Dkt. Joseph Daudi,
viongozi wa dini, mwenyekiti wa mtaa aliokuwa akiishi marehehu, ndugu wa
marehemu, serikali ya wanafunzi-IAASO na wanafunzi wote walihudhuria shughuli
hiyo.
Alipozungumza katika shughuli hiyo
ya kuaga mwili wa marehemu, Dkt. Grace Idinga amewatia nguvu familia, ndugu, jamaa
na marafiki ikiwemo wanafunzi wote wa IAA kwa kusema kuwa wasiwe na mawazo sana
juu ya kuondokewa na mpendwa wao, kwani ni safari na njia ambayo kila mmoja ataipita.
Aidha Dkt. Idinga amewasisitiza wanafunzi kuendelea na shughuli zingine ikiwemo
za elimu, na kuamini kuwa watatimiza malengo yao bali wasikae na kuwaza kuwa
nasoma halafu kumbe nitakufa.
Hata hivyo, Dkt. Idinga
aliihakikishia familia ushirikiano wa kutosha kutoka Chuo Cha Uhasibu
Arusha-IAA katika kusafirisha mwili wa marehemu kutoka Arusha hadi kufika
nyumbani Ruvuma-Songea kwaajili ya mazishi. Akisema kuwa IAA ina kampasi yake
Songea hivyo na Meneja wa kampasi hiyo amefika nyumbani kwa marehemu kwaajili
ya kushirikiana na familia na wanajamii katika shughuli ya mazishi.
Kwa upande wake Meneja wa
Kampasi ya Arusha Dkt. Joseph Daudi alizungumza namna alivyomfahamu mwanafunzi
Aneth Ndunguru wakati wa uhai wake, hususani akiwa mwanafunzi wa kampasi ya
Arusha, kuwa alikuwa ni mwanafunzi mwenye bidi katika masomo.
Naye rais wa Serikali ya
Wanafunzi-IAASO Francis Wambura amesema wanafunzi wameumizwa na kifo cha Aneth
Ndunguru, na hususani wanafunzi aliokuwa anasoma nao fani moja ya Utalii na
Ukarimu. Francis Wambura ameongeza kwa kuwasisitiza wanafunzi umuhimu wa
kujenga mahusiano mazuri na Mwenyezi Mungu kupitia kufanya ibada, kufanya
matendo mema wakati wote kwani kifo ni fumbo na haijulikani siku wala saa ya
kuja kwake.
Kila jambo linahitaji kumtanguliza
Mwenyezi Mungu, shughuli ya kuaga mwili wa marehemu Aneth Ndunguru ilihudhuriwa
pia na viongozi wa dini akiwemo Mchungaji Mathew Saganda kutoka kanisa la
SDA-Njiro. Mchungaji Mathew alitoa neno la Biblia lenye faraja na kutia
matumaini kwa jamii nzima iliyoguswa na kifo cha Aneth, akizungumzia kisa
kimoja cha mtu huko mashariki ya kati aliyepanda mti wake wa mzabibu akaumwagilia,
akautia mbolea na hakufaidi matunda yake. Basi akahusianisha na kifo cha Aneth
kuwa amesoma elimu zote lakini umauti umemfika akiwa Chuo Kikuu na kuwa Mwenyezi
Mungu amepanga na wakati wake umefika.
“Wewe leo unapumua, dada yetu
Aneth amepumzika hapo, ni kwa sababu huenda Mungu ameona huu mtini umetosha kunipatia matunda yanatosha matunda yake,
lakini wewe umebaki leo kwa sababu Mungu ana matarajio ya mabadiliko ya kuleta
matunda” Amesema.
Wanafunzi wa IAA waliokuwa wanasoma na marehemu Aneth Ndunguru wamemzungumzia kama mtu mwema, mwenye upendo, mwenye kushiriki kazi za kitaaluma na ushirikiano mbalimbali, wakisema hakika wataendelea kumkumbuka na wanamuombea mapumziko mema na Mwenyezi Mungu ampokee. Miongoni mwa wanafunzi waliomzungumzia Aneth ni Yusuph Kisabu na Lucia Range, wote wanafunzi waliokuwa wanasoma na marehemu Aneth Ndunguru.



